POLISI KISHAPU LATOA ONYO KWA MADEREVA WA SERIKALI KUELEKEA SIKUKUU

 

Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Insp. Rose R. Mbwambo, akitoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa magari ya Serikali wilayani humo Novemba 20,2026 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo

JESHI la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, limewataka madereva wa magari ya Serikali kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani, kufanya ukaguzi wa magari kabla ya safari na kuzingatia mwendo unaotakiwa ili kujikinga na ajali, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.


Wito huo umetolewa Novemba 20, 2026, na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kishapu, Inspekta Rose R. Mbwambo, wakati wa kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva wa magari ya Serikali katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.


Mbwambo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwakumbusha madereva umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani na kuwa makini wanapotumia magari, hususan kipindi cha mwisho wa mwaka ambapo watu wengi husafiri kwenda maeneo mbalimbali kwa ajili ya mapumziko na kusherehekea sikukuu.


Katika mafunzo hayo, madereva wamepatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya barabara, namna ya kuhuisha leseni za udereva, udereva wa kujihami pamoja na utunzaji wa vyombo vya moto na matumizi sahihi ya magari ya Serikali.


Aidha, wamekumbushwa umuhimu wa kukagua magari kabla ya kuanza safari, kuzingatia mwendo unaotakiwa na kuchukua tahadhari zote zinazolenga kulinda maisha yao, abiria na watumiaji wengine wa barabara.


Madereva hao wamepongeza jitihada za Jeshi la Polisi kuwafikia na kuwapatia elimu ya usalama barabarani, wakieleza kuwa yatawasaidia kuongeza umakini na uwajibikaji wanapokuwa barabarani. Aidha, wameeleza utayari wao wa kushirikiana na Jeshi hilo katika kutekeleza mipango mbalimbali ya pamoja ya kuimarisha usalama barabarani.


Jitihada hizo ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni na mikakati ya Jeshi la Polisi ya kuyafikia makundi mbalimbali ya watumiaji wa barabara, yakiwemo madereva, waendesha pikipiki, waendesha baiskeli , wasukuma mikokoteni na watembea kwa miguu, kwa lengo la kuwapatia elimu na kujenga utamaduni wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
 Transport Officer Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Benard Manyanya

Post a Comment

0 Comments