DKT MWIGULU- WAKUU WA MIKOA KUCHUKUA HATUA KALI KWA WAFUGAJI



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewaelekeza Wakuu wa Mikoa kuchukua hatua kali dhidi ya wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima bila ridhaa yao, akisisitiza kuwa wahusika wa makosa hayo wanapaswa kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria ili kudhibiti migogoro kati ya wakulima na wafugaji.


Akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea, Fadhili Ally Liwaka kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, Bungeni jijini Dodoma leo Novemba 5, 2026, Waziri Mkuu amesema hatua zichukuliwe dhidi ya mtu aliyefanya kosa badala ya kugeuza tukio hilo kuwa mgogoro kati ya jamii za wakulima na wafugaji.

“Kama mmoja amefanya kosa hilo, achukuliwe hatua kali huyo huyo. Wala wakulima wasione wafugaji ni adui zao, na wala wafugaji wasione wakulima ni adui zao,” amesema.

Amewataka wananchi kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutumia vyombo vya sheria kutafuta haki. Pia amewaelekeza viongozi kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuzuia ugawaji wa maeneo kinyemela, akitaja rushwa na matumizi mabaya ya ofisi kuwa miongoni mwa vyanzo vya migogoro.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuharakisha taratibu za kuuza mazao mara tu masoko yanapopatikana ili kuepusha kupoteza fursa za kibiashara kutokana na ucheleweshaji wa michakato ya mauzo.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kutafuta masoko ya kudumu na kupanua fursa za kuuza mazao nje ya nchi, huku akieleza kuwa bei ya ununuzi wa mahindi kupitia NFRA imeongezwa kutoka Sh. 450 hadi Sh. 500 kwa kilo.

Amewahimiza wakulima wenye mahindi wanayohitaji kuuza kufika katika ofisi za NFRA za mikoa na kanda ili kunufaika na bei hiyo iliyoboreshwa, akibainisha kuwa NFRA huenda isiweze kununua mahindi yote yanayozalishwa nchini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu katika Mkutano wa Tano, Kikao cha Nane cha Bunge la 13, jijini Dodoma.



Post a Comment

0 Comments