Mei 1,2026

Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Kuinusuru Stend United, Bw. Issa Mbaraka, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo akilalamikia kukwamishwa katika utekelezaji wa majukumu na kutofautiana kimalengo na wenzake.
Akizungumza na vyombo vya habari, Mbaraka amesema amefikia uamuzi huo mgumu baada ya kupitia changamoto nyingi zikiwemo vikwazo vya utendaji na mwelekeo tofauti wa wajumbe wenzake.
> "Rasmi naweka wazi kwamba mimi sio tena Mwenyekiti wa kamati hiyo maalum ya kuinusuru timu ya Stend United," alisema Mbaraka.
> "Nimefikia uamuzi huo baada ya kuona wengi niliokuwa nashirikiana nao katika kutekeleza majukumu hayo ni watu ambao siendani nao katika utendaji. Dhamira yangu ilikuwa ni kuiinusuru timu, lakini wenzangu walionekana kuwa na dhamira tofauti. Hali hiyo ilisababisha kupishana mara kwa mara."
Mbaraka amefafanua kuwa ameamua kung’atuka ili kulinda heshima yake binafsi, na kuwaacha wenzake waendelee na mipango yao.
> "Ili kulinda heshma yangu, nimeona niwaache waendelee na vile wanavyoviamini. Yote yatakayoendelea kwenye timu hiyo mimi sihusiki nayo," alisisitiza.
Kujiuzulu kwa Mbaraka kunazua maswali kuhusu hatma ya kamati hiyo na juhudi za kuinusuru Stend United, timu ambayo imekuwa ikikabiliwa na changamoto za kiuendeshaji na kifedha kwa muda sasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga, Said ManKilingo, amesema amepokea taarifa hizo kupitia vyombo vya habari na kumshauri Mbaraka kuwasilisha rasmi barua ya kujiuzulu ili kukamilisha taratibu.
ManKilingo ameongeza kuwa kama angepata nafasi ya kuzungumza naye kabla ya kufikia uamuzi huo, angeweza kumshauri na kusaidia kutafuta suluhu ya changamoto zilizokuwa zikikabili uongozi wa timu hiyo.
Naye Mjumbe wa mkutano mkuu TFF Kutoka Mkoa Wa Shinyanga Azan Saidi Mufti amesema kuamua kusaidia timu ya stend united ni kutokana na mtu binafs anavyopata msukumo wa kifanya hivyo kutokana na kuipenda timu na si kwa kulazimishwa vilevile amekili kutokuwa na taarifa za kujiuzuru kwa Mwenyekiti wa mpito wa timu hiyo.

0 Comments