SHINYANGA.
Na FLORA MASALU
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Himofilia Duniani pamoja na Chama cha Watu Wenye Ugonjwa wa Himofilia nchini, imeanzisha kliniki maalum katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi uliofanyika Aprili 21, 2026 katika hospitali ya Rufaa ya Shinyanga , Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Timoth Sosoma, alisema huduma hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kurahisisha matibabu kwa wagonjwa wa himofilia. Alifafanua kuwa hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali 16 nchini zilizoanza kutoa huduma za kliniki hiyo.
Sosoma alieleza kuwa upatikanaji wa dawa za himofilia zinazotolewa bure kupitia Shirika la Himofilia Duniani (WFH) ni hatua muhimu kwa taifa, kwani dawa hizo ni ghali lakini zina mchango mkubwa katika kuokoa maisha na kuzuia madhara makubwa ya ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa jitihada zimefanyika kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili kuongeza uelewa wa jamii na kuondoa dhana potofu zinazohusiana na ugonjwa huo.
"Tumefanikiwa pia kutoa mafunzo kwa wataalam wa tiba asili, maafisa afya ngazi ya jamii pamoja na wadau wa elimu wakiwemo walimu wakuu na maafisa elimu. Hii inalenga kuongeza uelewa mpana kwa jamii kuhusu ugonjwa wa himofilia na namna ya kuwahudumia wagonjwa,” amesema Sosoma.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kushiriki katika utoaji wa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa huo, akibainisha kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya kupunguza athari zake.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Himofilia Tanzania, Dkt. Abdallah Makalla, alisema kuwa juhudi za kupanua huduma zinaendelea kwa kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali. Alibainisha kuwa katika awamu ya tatu ya mradi, kliniki tatu tayari zimefunguliwa katika mikoa ya Singida, Geita na Shinyanga, huku mipango ikiendelea ya kufungua nyingine katika mikoa ya Ruvuma, Njombe na Lindi kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Dkt. Makalla pia alieleza kuwa mradi huo umeisaidia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kwa kuipatia vifaa muhimu vya matibabu, ikiwemo vitendanishi vya maabara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 1.5, vifaa vya tiba ya viungo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.5 pamoja na vifaa vingine muhimu.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Augustino Maufi, aliahidi kuwa wagonjwa wote watapata huduma bora na ya kitaalamu.
"Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na friji maalum kwa ajili ya kuhifadhia dawa za wagonjwa wa Himofilia, friji kwa ajili ya huduma za fiziotherapia, kompyuta kwa ajili ya kutunza kumbukumbu za wagonjwa, pamoja na vitendea kazi vingine vya zaidi ya shilingi milioni saba,”amesema Dkt. Maufi.
Baadhi ya wagonjwa walioshiriki katika tukio hilo walieleza kuwa kuanzishwa kwa kliniki hiyo kumewapa matumaini mapya ya kupata huduma kwa wakati na kuepuka madhara yatokanayo na ugonjwa huo.
Himofilia ni nini?
Himofilia ni ugonjwa wa kurithi wa damu unaosababisha mwili kushindwa kugandisha damu kwa kawaida kutokana na upungufu wa vinasaba vya kugandisha damu (clotting factors). Hali hii hupelekea damu kuvuja kwa muda mrefu kuliko kawaida au kutokwa damu ndani ya mwili.
Hata hivyo, takribani asilimia 30 ya wagonjwa hupata himofilia bila kurithi (sporadic hemophilia), hali inayotokana na mabadiliko ya vinasaba (gene mutation) yanayotokea bila historia ya ugonjwa katika familia.
Mtu mwenye himofilia huishi na ugonjwa huu maisha yake yote, kwani hauponi kabisa, lakini unaweza kudhibitiwa kwa matibabu sahihi na ya mara kwa mara ili kuzuia madhara makubwa.
Dalili za himofilia ni pamoja na kutokwa na damu ndani ya mwili bila jeraha la wazi, hasa kwenye ubongo, misuli au maungio, pamoja na kuvimba na maumivu kwenye viungo kutokana na damu kuvuja ndani. Vilevile, mgonjwa anaweza kupata kutokwa na damu kwa muda mrefu isivyo kawaida baada ya kupata jeraha, pamoja na kutokwa na damu nyingi baada ya kufanyiwa upasuaji au kung’olewa jino.




0 Comments